Ndugu wa mume wa UFOO SARO wapinga madai kwamba ALIJIUA.....Je, kibao cha mauaji kitamgeukia Ufoo Saro???...Tusubiri Uchunguzi

Imeandikwa na JESSICA
KILEO, Gazeti la Uhuru 
FAMILIA ya aliyekuwa mzazi mwenzake, Mwandishi
wa ITV na Radio One, Ufoo Saro, Anthery Mushi (40), imevunja ukimya na
kudai inapata wakati mgumu kuamini kwamba ndugu yao alijiua
mwenyewe. Imesema suala hilo inaliachia Jeshi la Polisi lishughulikie
ili kubaini undani wake.
Kaka wa marehemu, Isaya Mushi alidai
hayo jana alipozungumza na waandishi wa habari katika Hospitali ya Taifa
 Muhimbili (MNH), wakati mwili wa Mushi, aliyejiua kwa kujipiga risasi
 na kumuua mama mkwe wake, Anastazia Saro pamoja na kumjeruhi mchumba wake Ufoo, ukiagwa.
Mushi
 alidai wapo katika wakati mgumu wa kuamini kwamba ndugu yao alijiua
mwenyewe, kwani haiwezekani mtu akajipiga risasi sehemu mbili ambazo ni
kidevuni na upande wa bega la kushoto.

Alidai sio kazi yao kutoa hukumu, kwani wanasubiri upelelezi wa polisi kutoa jibu lililo sahihi kuhusiana na tukio hilo.
"Baada
 ya kifo cha ndugu yetu, wanafamilia tulifanya uchunguzi wa awali na
bado linatuwia vigumu kutambua upi ni ukweli kuhusu jambo hilo kuhusiana
 na kifo hiki," alidai.

Kaka huyo alidai katika uchunguzi wa madaktari, walibaini kuwa marehemu alijipiga risasi mbili sehemu tofauti.Akisoma
 risala kwa waombelezaji, Mushi alidai marehemu alizaliwa Januari 3,
1973 katika kijiji Uru Ongoma Timbirini wilayani Moshi mkoani
Kilimanjaro. Alisoma Shule ya Msingi Ongoma Timbirini kutoka mwaka 1981
hadi 1987 na alijiunga na Shule ya Sekondari ya Zanzibar na baadaye
alisoma kozi mbalimbali, ikiwemo uandishi wa habari.  Mwaka 1994
alijunga na Kituo cha Televisheni cha ITV na mwaka 2002 alikwenda STR na
 hadi mauti inamkuta alikuwa akifanya kazi Umoja wa Mataifa, Sudan,
akiwa mtaalamu wa habari.

Dada wa marehemu, Eviolatha Mushi
alisema alipokea kwa masikitiko msiba wa mdogo wake kwa sababu alikuwa
mtu mwelewa na msikivu katika jamii ambayo wamekulia.
Eviolatha alitoa
wito kwa wanandoa kumshirikisha Mungu katika maisha yao na sio
mwanadamu, hali itakayosaidia kutatua matatizo wanayopitia kwa kuwa neno
 la Mungu linasema kila mwanadamu aliyezaliwa na mwanamke lazima
atalamba mauti, hivyo hawana budi kukubaliana na neno hilo.
Mdogo
 wa marehemu, Happy Mushi, alisema hadi sasa hawezi kuamini chochote
hadi polisi itakapotoa majibu ya upelelezi. Alisema Oktoba 9, mwaka huu,
 marehemu alimpigia simu na kumwambia anamshukuru Mungu, kwani ametoka
kufanya kazi katika mazingira magumu, hivyo muda si mrefu anaweza
kuhamia Tanzania, na kwamba yupo nchini kwa ajili ya kumalizia nyumba
yake ambaye ipo Mbezi, Dar es Salaam.
Lakini cha kushangaza kabla ya
wiki alisikia katika vyombo vya habari vikitangaza kaka yake amejiua
mwenyewe pamoja na familia ya mke wake,' alisema.
Mwili wa marehemu ulisafirishwa jana kwenda kijijini kwao Ongoma Timbirini na unatarajiwa kuzikwa leo.
Wakati
 huo huo, Ufoo aliyelazwa Muhimbili hali yake imetengemaa na ameanza
kutembea pamoja na kwamba daktari anayemhudumia anakataza watu kuingia
kumtazama.
Ofisa wa Habari wa MNH, Aminiel Eliegaisha, alisema
jana kuwa, Ufoo anaendelea vizuri na ameanza mazoezi ya kutembea, ingawa
 bado hawajaanza kuwaruhusu watu kwenda kumtaza kwa sababu ameshonwa
sehemu nyingi na kwamba wanahofia kidonda kutokupona haraka.
Tukio
 hilo la mauaji lilitokea Oktoba 13, mwaka huu, eneo la Kimbamba
nyumbani kwa wazazi wa Ufoo, ambapo alikwenda akiwa na mzazi mwenzake
Anthery Mushi. Iliripotiwa kuwa Mushi alimuua mama wa Ufoo kwa kumpiga
risasi zinazosadikika tano na kumjeruhi kabla ya kujiua mwenyewe

0 comments:

Post a Comment

Recent Posts