NAIBU WAZIRI WA AFYA WA ZAMANI LUCY NKYA ADAIWA KURUSHIANA RISASI NA MWANAE, MWANAE AKANUSHA

Dk. Lucy Nkya

Kumekuwepo na taarifa kuwa aliyewahi kuwa Naibu Waziri wa Afya Dk. Lucy Sawere Nkya na mbunge wa jimbo la Morogoro Kusini Mashariki na mwanae wa kiume Jonas Nkya wamerushiana risasi za moto kwenye ofisi yake mjini Morogoro kwa kile kilichodaiwa kimetokana na ‘Mzozo wa Kifamilia.’
Hata hivyo akiongea na kituo cha runinga cha ITV jioni hii, Jonas ambaye ni Mwenyekiti wa umoja wa vijana wa CCM Mkoa wa Morogoro, amekanusha taarifa hizo na kudai kuwa bunduki aliyokuwa nayo ilijipiga kimakosa.
“Ni uongo tu ndugu mtangazaji ni uongo na sijui imekuwa vipi mpaka imefika hapo lakini sio kweli,” amesema Nkya. “Ni kitendo tu hiyo risasi ilivyojifyatua hapo Faraja wala mama mwenyewe hakuwepo ofisini. Sijui hata mama mwenyewe silaha hana. Kwahiyo hatuwezi kurushiana risasi lakini tatizo ni kwamba hapa kuna polisi, kuna majirani, kuna nyumba za watu baada ya risasi kujipiga wakapaniki, sasa sijui kwanini wamefika stage ya kurushiana risasi mimi na mama yangu, sio ukweli,” ameongeza.
Jonas Nkya
“Nilikuwa naye pamoja tumeamka pamoja na mimi nimemuaga amekwenda kwenye shughuli zake mimi nimeenda kubadilisha gari niende shamba, tuna utaratibu kila Jumamosi ninaenda shamba kwahiyo hicho ndicho kilichotokea hakuna! Hata mimi nimeanza kupata hizi habari nipo shamba nimerudi hapa nakutana na waandishi wa habari tena barabarani, hakuna kitu kama hicho.”
Akizungumzia jinsi risasi ilivyofyatuka alisema:
“Kwanza ni kitu ambacho kimenishitua, kwanini wamemuingiza mama kwenye suala kama hilo? Kwa sababu ilikuwa ni nje na mama alikuwa hayupo, yupo ndani ofisini kwake, sasa kama tungerushiana risasi ingekuwa ofisini kwake! haikuwa hivyo. Hii silaha inakaa kiunoni na mimi natoka kwenye gari dogo naingia kwenye gari na ikaanguka kupitia mguu wangu wa kulia na risasi yenyewe ya kizamani ikajipiga risasi moja ambayo ilikuwa kwenye chamber, moja tu! Sasa baada ya kusikia na wakaona hamna kitu wakaondoka, sasa baadaye huku nyuma ndo ninaanza kupigiwa masimu kwamba kuna habari kama hiyo, sijui tulikuwa kwenye kikao, wengine wanasema nilikuwa naumwa malaria sijui! Sielewi kwakweli, sielewi!”
“Lakini ukweli ndo huu nakwambia, hapo ofisini kulikuwa kuna mlinzi, hapo ofisini kuna wafanyakazi leo jJmamosi kulikuwa hakuna watu wengi, halafu nilikuwa na dereva wangu pia, mwana James alikuwa yupo, wanamfahamu na nimeshawaambia wanaweza kumuuliza! Pia nimewaambia wakamtafute mama, sema mama mwenyewe yupo na kazi zake kwahiyo nimewaomba ili kupata vizuri ukweli wakamuone atawaeleza, hakuna habari kama hiyo,” alisisitiza Jonas.
Jonas amekanusha uvumi kuwa yeye na mama yake hawaelewani.
“Hapana hapana mimi na mama yangu nipo naye vizuri, tunaishi pamoja kwa sababu ya kumsaidia baba yetu. Leo asubuhi tumeamka naye, tumeongea, tumeagana, yeye anakwenda na shughuli zake mimi nakwenda shamba tumetoka nyumba moja! Kwahiyo kama ugomvi ungefanyika nyumbani sio ofisini. Kwahiyo nataka kusema ukweli hizo taarifa hakuna ukweli hata kidogo.
Jonas amewaasa wananchi kutoamini kwa haraka habari wanazozisoma mtandaoni bila kufanya uchunguzi.
“Cha kwanza nataka kuwaambia ni uongo, lakini pia naomba jamani hao wenzetu wawe makini na social media. Kwanza wawe wakweli na cha msingi tusichafuane kabisa. Kama kuna mambo ya siasa haina haja, tusichafuane kiasi hicho! Obvious jiulize kwanini mama hakuwepo, halafu wanasema nilikuwa nataka kumpiga mama yangu,” alihoji.
Hakuna taarifa hadi sasa iliyotolewa na Mama Lucy Nkya.

0 comments:

Post a Comment

Recent Posts