JINSI YA KUTAMBUA FURSA NA KUWEZA KUANZISHA BIASHARA YAKO BINAFSI.

Je utawezaje kutambua fursa na kuweza kuanzisha biashara katika mazingira yako? Bila shaka hili swali watu wengi wanaotamani kumiliki biashara zao binafsi wamekuwa wakijiuliza mara kwa mara pasipo kutilia msisitizo katika maisha yao. Unaweza kufikiri mambo mengi sana kuhusu namna ya kuwa na biashara yako binafsi lakini kutokuwa na nia madhubuti ni sababu kuu inayokufanya usite na hata kupoteza utayari wako wa kutaka kumiliki biashara yako binafsi.

Kwanza kabisa ni muhimu ujue FURSA maanake ni nini hasa, kwa ufafanuzi rahisi FURSA ni uwezo wa mtu kutambua nafasi/bahati yenye manufaa kwake kulingana na kile alichoazimia kupata au kufanikiwa. Fursa zipo tele ila huwezi kuona fursa ikiwa hujaazimia kufanya lolote hata kama utapata nafasi ya kutumia fursa yenyewe au ikiwa huna malengo yeyote yale.

JE UTAWEZAJE KUONA AU KUTAMBUA FURSA?

Utaweza kuona fursa ikiwa tayari ulishakuwa na malengo ya kufanya biashara yenyewe. Ninachomaanisha ni kwamba kuwa na mpango wa kufanya biashara kabla kuanzisha biashara yenyewe ndio njia pekee ya kuweza kuona fursa itakayojitokeza mbele yako kwakuwa tayari ulishakuwa na mawazo ya fursa hiyo.

Mfano: Katika mtaa unaoishi kuna shughuli nyingi za ujenzi zinaendelea. Kutokana na shida ya upatikanaji wa vifaa na vitu vingine vya ujenzi kama simenti, mbao, tiles, mabati nakadhalika.
Kwasababu ulishakuwa na wazo la biashara ya Hardware Shop ama kwa kusikia au kuona kwa mtu mwingine ambaye tayari anafanya biashara hiyo ya Hardware Shop labda mahali pengine. Ni rahisi kwako kuona fursa ya kuanzisha Hardware Shop yako mwenyewe katika mtaa wako kwa kuwa tayari ulishakuwa na wazo hilo.

Hatimaye utakavyoweza kuona fursa utaweza kuamua kuwasogezea huduma watu wa mtaani kwako kwa kufungua duka kubwa la Vifaa Vya Ujenzi (Hardware Enterprise). Pia kwakuwa mahitaji ya vifaa vya ujenzi ni makubwa, unapanga bei nakuuza bidhaa zako kwa bei poa na watu wa mtaani kwako watamiminika kununua bidhaa zako zilizo bora kabisa.

Tumia hizi mbinu 5 nilizoziorodhesha zikusaidie katambua fursa.

1. Tafakari biashara yoyote ile unayopenda kufanya. (Tafakari bila kufikiria ugumu wa kuanzisha biashara yenyewe)

2. Andika chini kwenye karatasi na orodhesha mambo muhimu yanayohitajika kuanzisha biashara yenyewe. (Orodhesha kwenye karatasi biashara nyingi uwezevyo kwa kadri utakavyofikiri)

3. Kati ya biashara ulizoorodhesha, fikiri katika maeneo yako ni biashara gani imekamata soko kwa wakati huo.

4. Kati ya hizo biashara ulizooresha kwenye karatasi, jiulize je ni biashara ipi kati ya hizo ulizozitaja ungependa ufanye?

5. Kisha andika mambo yote utakayohitaji kufanikisha kuanzisha biashara hiyo mfano: Kutathmini kiasi cha mtaji unachohitaji, mfanyakazi au idadi ya wafanyakazi wa kukusaidia nakadhalika.

Zingatia hayo mambo matano hakika utafungua maono yako na kuweza kuona fursa, pia jitahidi sana kuamini kuwa UNAWEZA kuanza biashara yako binafsi na kujiajiri mwenyewe. Kikubwa jipange kwa kutumia hizo mbinu 5 nilizokupatia, ukishakuwa tayari usiogope kuchukua hatua nyingine ya kutafuta mtaji wa kukuwezesha kufungua biashara yako na hakika ukithubutu kujaribu utafanikiwa.

0 comments:

Post a Comment

Recent Posts