Viongozi Chadema wazipiga kavukavu kwenye mkutano wa Mbowe
Mkutano wa Baraza la Uongozi la Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema) Kanda ya Kaskazini juzi uligeuka ukumbi wa ngumi,
baada ya Mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba
kushushiwa kipigo.
Mwigamba alishushiwa kipigo hicho na baadhi ya
viongozi wenzake wa chama kwa madai ya usaliti na tayari amesimamishwa
uongozi kwa muda usiojulikana.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas
jana alithibitisha kutokea kwa vurugu hizo na viongozi hao wa Chadema
kufikishana polisi.
Alikutwa na zahama hiyo mbele ya viongozi wakuu
wa Chadema Taifa, Mwenyekiti, Freeman Mbowe na mwasisi wa chama hicho,
Edwin Mtei katika Hoteli ya Coridal Spring.
Viongozi hao wamekuwa wakifanya ziara za aina hiyo
nchi nzima, kuimarisha chama na kujipanga kwa ajili ya uchaguzi wa
Serikali za Mitaa mwakani na uchaguzi mkuu ujao wa Rais na wabunge mwaka
2015.
Habari kutoka ndani ya mkutano huo zinaeleza kuwa
hatua hiyo ilifuatia tuhuma kwamba Mwigamba alituma ujumbe kwenye
mtandao wa kijamii wa Jamii Forums, unaodaiwa kukichafua chama hicho.
Tukio hilo la aina yake lilitokea wakati viongozi
wote wa juu wa chama hicho, wakiongozwa na Mbowe walipokuwa wakijadili
mustakabali wa chama hicho, mkutano ambao ulihudhuriwa na wabunge karibu
wote wa Chadema wa kanda hiyo.
Hata hivyo, wakati mijadala ikiendelea baadhi ya
viongozi wa chama hicho, akiwamo Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini,
Godbless Lema walimtuhumu Mwigamba kutuma ujumbe kwenye mtandao huo,
uliokuwa ukizungumzia ufisadi ndani ya chama hicho, wakidai alitaka
Mwenyekiti Mbowe kukubali kuchunguzwa.
Akizungumza na Mwananchi Jumapili jana, Mwigamba
alisema kuwa baada ya Lema kutoa tuhuma hizo aliungwa mkono na viongozi
wengine na vijana waliokuwa wameimarisha ulinzi, kumvamia na kuanza
kumpiga pamoja na kumnyang’anya kwa nguvu kompyuta mpakato (Laptop),
aliyokuwa nayo, kisha kumpeleka Kituo Kikuu cha Polisi, mjini Arusha.
“Wamenipiga sana na kuniweka ndani, ila nashukuru
Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya Arusha (OCCID), alikuja na kunitoa saa
5:00 asubuhi,” alisema Mwigamba.
Alisema kuwa leo katika mkutano wake na waandishi
wa habari ataeleza yote yaliyotokea na hatua atakazochukua, kwa kuwa
yeye ni kiongozi wa juu wa chama.
Hata hivyo, alieleza kwamba bado anashauriana na wanasheria wake kuona kama anaweza kuwachukulia hatua waliompinga.\
Kauli ya polisi
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas
alisema polisi wameona hakuna kosa la kisheria lililotokea hasa kutokana
na malalamiko yaliyofikishwa kwao dhidi ya Mwigamba ya kukichafua chama
kwenye mitandao.
“Hili suala la mitandao ni kubwa na lina taratibu
zake sasa kusema tu umechafuliwa na iwe kesi nadhani uchunguzi
unahitajika kwao, sisi tumeona haya ni mambo yao wanaweza kuyamaliza wao
ndiyo sababu tulimwachia, Mwigamba,” alisema Sabas.
Kosa analodaiwa kufanya Mwigamba
Akizungumzia sakata hilo jana, Mbunge wa Arusha
Mjini, Godbless Lema alisema kwamba Mwigamba alibainika kutuma
ujumbe kwenye mtandao wa Jamii Forums uliokichafua chama hicho, akieleza
haikuwa mara yake ya kwanza kwa kiongozi huyo kufanya hivyo na kwamba
walikuwa wakimfuatilia kwa muda mrefu.
“Kilichotokea ni hicho, vijana wa Red Brigade
ndio waliomtoa ukumbini, baada ya kumbaini kukichafua chama, kwani
laptop yake baada ya kuchunguzwa na wataalamu wetu walijiridhisha ni
yeye ndiye aliyetuma ujumbe huo,” alisema Lema.
Katibu wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Amani
Golugwa alitaja tuhuma zinazomkabili Mwigamba kuwa ni pamoja na kusema
uongo, kupotosha taarifa za chama na kuchonganisha viongozi kupitia
mtandao wa kijamii ya Jamii Forums.
Katika andiko lake kwenye mtandao, Mwigamba
anadaiwa kuwatuhumu viongozi wa juu wa Chadema akiwamo Mwenyekiti wa
Taifa, Freeman Mbowe na Katibu Mkuu, Dk Wilbrod Slaa kuwa wamechakachua
katiba ya chama hicho kuhusu ukomo wa nafasi za uongozi ili kujinufaisha
binafsi.
Golugwa alisema kuwa baada ya kubanwa kwenye
kikao, Mwigamba alikiri kuandika na kurusha taarifa hizo kwenye
mitandao, lakini alipotakiwa kukabidhi kompyuta yake ili ichunguzwe na
wataalamu wa mawasiliano wa chama hicho aligoma, hali iliyozua tafrani
kati yake na walinzi wa chama hicho (Red Brigade), waliolazimika kutumia
nguvu kumdhibiti.
Purukushani zilivyotokea
Habari zaidi zinaeleza kuwa katika harakati za
kutaka kumnyang’anya Mwigamba kompyuta yake, mwenyekiti huyo wa Chadema
mkoani Arusha alianza kushambuliwa na baadhi ya viongozi wa Chadema,
kabla ya kufanikiwa kumdhibiti.
Zinaeleza kuwa katika tukio hilo kulitokea pia
kurushiana maneno na matusi ya nguoni kati yake na viongozi wengine wa
chama hicho akiwamo Lema.
Baadaye Lema aliliambia gazeti hili kwamba katika purukushani hizo Mwigamba alimrushia ngumi ambayo hata hivyo aliikwepa.
Alisema kuwa wanakusudia kumfungulia kesi Mwigamba ya kukichafua chama chao katika mitandao ya kijamii.
Hata hivyo, alisema kikao chao kiliendelea jana
bila ya vurugu zozote na kuweka mikakati ya kushinda majimbo yote ya
Kanda ya Kaskazini mwaka 2015 na kuchukua nchi katika uchaguzi huo ujao.
Adhabu kwa Mwigamba
Katika hatua nyingine Chadema, kimemsimamisha
uongozi Mwigamba kwa tuhuma za kukisaliti, kukihujumu chama hicho na
viongozi wake.
Akitangaza uamuzi huo mbele ya waandishi wa habari
jijini Arusha jana, Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Israel
Natse alibainisha kuwa uamuzi wa kumsimamisha Mwigamba katika nyadhifa
zote za uongozi ndani ya chama ulifikiwa na kikao cha Baraza la Uongozi
wa Kanda ya Kaskazini kilichokutana juzi.
Alisema kuwa Mwigamba amesimamishwa kwa muda
usiojulikana kupisha uchunguzi wa tuhuma dhidi yake na kuonya kuwa iwapo
tuhuma zitathibitishwa, hatua nyingine za kinidhamu zitafuata kulingana
na kanuni na katiba ya Chadema.
“Kwa sasa Mwigamba anatuhumiwa kuvunja sura ya
kumi, kifungu cha 10.1 kifungu kidogo cha 8, 9 na 10 ya katiba ya
Chadema inayozungumzia maadili ya uongozi,” alisema Natse.
Akifafanua zaidi alisema kuwa sura na vifungu
hivyo vinakataza kiongozi wa chama hicho kutoa tuhuma dhidi ya viongozi
wenzake bila kufuata vikao halali vya kikanuni na kikatiba.
MWANANCHI
MWANANCHI
0 comments: