SERIKALI YAWEKA MSIMAMO KUTENGWA KUTENGWA EAC

Serikali imeshaanza kuchukua hatua baada ya nchi za Rwanda, Kenya na Uganda kutoihusisha katika mambo yanayohusu Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), ikiwa ni pamoja na kutohudhuria mikutano ya jumuiya hiyo yenye ajenda ambazo nchi hizo tatu zimekwishaweka msimamo wa peke yao.
Nchi za Rwanda, Uganda na Kenya zimeanzisha ushirikiano wa pamoja katika maeneo ya miundombinu, biashara na viza ya pamoja na mara nyingi viongozi wakuu wa nchi hizo wamekuwa wakifanya mikutano bila kuihusisha Tanzania na Burundi.
Serikali jana kupitia kwa Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta ilitoa ufafanuzi huo bungeni, baada ya wabunge kutaka ieleze msimamo wake kuhusu suala hilo. Katika swali lake la nyongeza, Mbunge wa Same Mashariki (CCM), Anne Kilango alitaka kujua msimamo wa Serikali baada ya kuwepo kwa dalili za kuvunjika kwa jumuiya hiyo.
Katika ufafanuzi wake, Sitta alisema: “Si kwamba Serikali imekaa kimya, kuna mambo mengine yanaendelea. Tumeanza kuchukua hatua kuonyesha kuwa hatuwezi kuendelea na hali hii inayofanana na mchezo wa kuigiza.”
Sitta alisema kuwa hivi sasa Serikali haitashiriki katika mikutano ya jumuiya hiyo ambayo ajenda zake zinahusu mambo ambayo nchi hizo tatu zimekubaliana peke yao. “Kuna mkutano jijini Nairobi unaowahusisha mawaziri wa mambo ya nje, mamlaka kuu imeamua kwamba waziri wetu wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe asihudhurie,” alisema Sitta na kuongeza:
“Kama tunazungumza sera ya mambo ya nje na wenzetu wanataka kuunda shirikisho bila kutushirikisha, haitakuwa na maana sisi kwenda kukaa katika vikao ambavyo hayo yanayozungumzwa wao tayari wamekwishayawekea msimamo.”
Alifafanua: “Tunachukua hatua na hatushiriki katika vikao vyao, kama wao wamekubaliana, basi haipo sababu ya sisi kwenda. Tunaitazama hali hii siku hadi siku.”
Alisema kuna mkutano unafanyika Burundi leo, Serikali imemwagiza Naibu Waziri wa Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Abdullah Abdullah kutohudhuria, kwa maelezo kuwa ajenda za mkutano huo zinahusu mambo ambayo tayari nchi hizo zimekubaliana.
“Katibu Mkuu wa Wizara ya Afrika Mashariki anaondoka leo (jana) kwenda kuhudhuria mkutano huo. Tumetoa ushauri kwa watendaji wa Serikali wanaohudhuria vikao ambavyo wanasiasa hawapo, wasitoe msimamo wowote wa nchi, bali wasikilize na kuja kutueleza,” alisema.
Alisema mpaka sasa Tanzania inatafuta ufafanuzi wa suala hilo Makao Makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, kwamba baada ya wiki mbili yatatolewa majibu na Tanzania itachukua hatua.
Awali, katika maswali ya nyongeza Mbunge wa Mbinga Magharibi (CCM), John Komba alihoji kwa nini Tanzania hailaani nchi hizo kuanzisha jumuiya ndani ya jumuiya, huku akipendekeza Tanzania iunde jumuiya mpya itakayozihusisha nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Burundi.
Mbunge wa Wawi (CUF), Hamad Rashid Mohamed alitaka kujua msimamo wa Tanzania kiuchumi iwapo jumuiya hiyo itavunjika, huku akieleza kuwa tayari Kenya imekubaliana na Ethiopia na Sudan kwa ajili ya kutumia nchi hizo kibiashara.

Mbunge wa Viti Maalumu (CUF), Rukia Ahmed alitaka ufafanuzi wa Tanzania kuendelea kutengwa katika jumuiya hiyo kwa kuwa hatua hiyo ni kinyume na makubaliano ya mkataba wa ushirikiano huo.
Mbunge huyo alisema hata Waziri Membe amewahi kukiri kuwa Tanzania inasubiri talaka kutoka katika umoja huo.
Akijibu maswali hayo, Sitta alisema: “Hawajaanzisha shirikisho, bali wapo katika harakati fulani ambazo mwisho wake hatuujui. Ikifika mahali wakakubaliana tutajua uamuzi wa kuchukua. Kwa sasa ni mapema mno kuchukua hatua wakati wao wakiwa katika maandalizi.”
Sitta alifafanua kuwa nchi nyingi barani Afrika zinakumbwa na sintofahamu na migogoro kwa sababu ya kauli na uamuzi kutoka viongozi wake, huku akihoji: “Hivi mnajua kwa nini Rwanda wanatununia?”
Aliongeza, “Nchi kama Rwanda, Burundi na Tanzania zitaendelea kuwapo. Tusichukue hatua wakati ambao nchi fulani zinaleta uchokozi, matokeo yake sisi ndiyo tutaharibu zaidi.”
Alisema hali hiyo ndiyo inaifanya Tanzania kushindwa kuchukua hatua za kulaani vitendo vinavyofanywa na nchi hizo, na kuwa Serikali itakapojiridhisha na matukio yanayofanywa na nchi hizo wabunge watataarifiwa na hatua itakayochukuliwa itakuwa yenye kulinda masilahi ya Tanzania.
Alisema Serikali haiwezi kuchukua hatua kutokana na kuwepo kwa dalili fulani, lakini pamoja na hilo, hiyo haina maana kwamba Tanzania haijiandai kwa ajili ya mazungumzo na ushirikiano na Burundi na DRC. Alisema kibiashara Tanzania inafaidika zaidi na DRC na sio Burundi wala Rwanda: “Rwanda wanatugusa kwa sababu barabara ya lami tuliyojenga kwenda Rusumo inapita Rwanda ili kufika Goma, DRC na hapo ndipo inapokuja shida kidogo.”
Aliongeza kwa kusema, Serikali inaharakisha ujenzi wa reli kutoka Uvinza mkoani Kigoma kwenda Msongati ili kuikoa Burundi.
“Kutoka Mji Mkuu wa Burundi, Bujumbura mpaka Bandari ya Mombasa, Kenya ni mbali. Wakitumia bandari hiyo umbali unaongezeka kwa kilomita 900 ikilinganishwa na umbali kutoka Bujumbura hadi Dar es Salaam.”
Sitta alisema inakera kuona nchi hizo zikiizunguka Tanzania, huku akiwataka wabunge kufuata ushauri wa Rais mstaafu, Ali Hassan Mwinyi.
“Katika mazingira yanayofanana na haya, Rais Mwinyi aliasa kwamba muongo muongoze. Maana yake ni hivi, kama wenzetu wana hila haitachukua muda tutazibaini tu,” alisema na kuongeza:
“Jana (juzi) wamekutana tena kule Kigali Rwanda, lakini sisi kwa sababu tumeshamuhoji mwenyekiti wetu wa
Hata hivyo, Sitta alionya: “Kama utaendelea uongo wa kitoto, Serikali hii ni makini, tutakuja bungeni na tutaweka mapendekezo, lengo likiwa ni kukabiliana na hali hii ya kuchezewa chezewa.”
Sitta alisema Tanzania haijaolewa na nchi wanachama wa jumuiya na kufafanua kuwa Tanzania ni asilimia 52 ya eneo zima la nchi zilizopo katika jumuiya hiyo, “Nadhani sisi ndiyo waoaji na hatuwezi kusubiri talaka, kama ni talaka tutaitoa sisi.”
Baraza la Mawaziri, baada ya wiki mbili tuna kikao basi tusubiri tutakachoambiwa.”

0 comments:

Post a Comment

Recent Posts