KAPT KOMBA AJITOA MHANGA ASEMA LOWASA NDIYE RAIS 2015
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Kapteni Mstaafu, John
Komba amevunja ukimya na kutamka wazi kuwa Waziri Mkuu wa zamani,
Edward Lowassa, ndiye chaguo lake na atakuwa Rais ajaye uchaguzi wa
2015.
Komba anakuwa mtu wa pili kumtaja Lowassa hadharani kuwa anafaa kwa rais 2015.
Itakumbukwa Mbunge wa Viti Maalumu, Beatrice
Shelukindo (CCM) naye alivunja ukimya baada ya kutangaza kumuunga mkono
Lowassa kumrithi Rais Kikwete.
Shelukindo alitoa kauli hiyo wakati akiwasalimia
wakazi wa Monduli baada ya kukaribishwa kuchangia ujenzi wa Hosteli ya
KKKT, kwenye sherehe za kukaribisha Mwaka Mpya zilizofanyika nyumbani
kwa Lowassa na kuhudhuriwa na makada kadhaa wa CCM.
Akizungumza na Mwananchi katika mahojiano maalumu
jana, Komba ambaye ni Kiongozi wa Kundi la Uhamasishaji cha CCM Tanzania
One Theatre (TOT Plus), alisema mtazamo wake kwa mtu anayefaa kumrithi
Rais Jakaya Kikwete ni Lowassa.
Komba aliyeingia kwenye siasa kutokana na msukumo
wa mama yake aliyekuwa msaidizi wa Bibi Titi Mohamed, alisema anazo
sababu kuu tano za kumkubali Lowassa kuwa Rais na atasimama popote
kumtetea.
“Nakuambia Lowassa ndiye anafaa kuwa Rais... unafikiri kuna mwingine. Nina sababu zangu tatu,” alisema Komba na kuhoji:
“Wewe unakwenda kwenye harambee, nani leo hii
anaweza kusaidia kuchangia kwa fedha nyingi na zote hizo ni kwa
maendeleo yanayokusudiwa kama siyo Lowassa?”
alisema Komba ambaye ni mahiri katika kuinadi CCM,
katika kampeni mbalimbali za udiwani, ubunge na urais.Juu ya kuwa
atakuwa katika wakati mgumu endapo anayempigia debe hatokuwa, Komba
alisema: “Mimi sikwambii ni nani, lakini wapo Mawaziri waliomkana,
lakini leo hii wapo kwenye Serikali hii hii ya Rais Kikwete.
“Mimi nasema Lowassa, na kama akipita sawa
nitaburudiiika kwelikweli, lakini kama akiteuliwa mwingine, mimi
nitakuwa naye...nitamwimbia hadi mwisho. Kazi yangu si unaijua,
nitampigia debe kwa kuwa si mtu wa mtu mmoja, ni uteuzi wa wanaCCM ule
si wa Komba.” alisema.
Mbali na kumnadi Lowassa, Komba alisifu uimara wa
chama chake kuwa kinaimarika siku hadi siku na ndicho kinachotoa
viongozi wa kweli na hata wananchi wanakikubali.
Akizungumzia suala la rushwa ndani ya CCM, Komba
ambaye pia ni Mbunge wa Mbinga, alisema kama chama kuna watu wa aina
nyingi, kuna wasafi, kuna wachafu lakini wote wako kwenye mstari mmoja.
Alisema kuwa vita ya rushwa ndani ya CCM itamalizika endapo kila kiongozi atasimamia kwenye haki na maadili ya uongozi na pia kutambua wajibu wake ndani ya chama.Komba alijipigia upatu kuwa ameleta maendeleo katika jimbo lake kwani jimbo linatazamika ikilinganisha na miaka ya nyuma kuwa wananchi walikuwa wakiishi maisha ya tabu na kimaskini ilhali wana raslimali za kutosha.
Alisema kuwa vita ya rushwa ndani ya CCM itamalizika endapo kila kiongozi atasimamia kwenye haki na maadili ya uongozi na pia kutambua wajibu wake ndani ya chama.Komba alijipigia upatu kuwa ameleta maendeleo katika jimbo lake kwani jimbo linatazamika ikilinganisha na miaka ya nyuma kuwa wananchi walikuwa wakiishi maisha ya tabu na kimaskini ilhali wana raslimali za kutosha.
0 comments: