Ni mkakati wa kuiengua Tanzania kutoka EAC?
Tangu Rais Jakaya Kikwete alipotoa ushauri kwa nchi ya Rwanda kukaa na waasi wa FDLR ili wamalize migogoro yao, uhusiano baina ya Tanzania na Rwanda umekuwa shakani.
Mwaka 1994, wanajeshi wa Kihutu na wanamgambo waliua watu 800,000 nchini Rwanda wengi wao wakiwa Watutsi.
Kwa sasa, Rwanda inatawaliwa na Serikali ya Watutsi chini ya Rais Paul Kagame, huku makundi ya kijeshi ya Kihutu yakifuatilia kwa mbali. Moja ya makundi hayo ni FDLR.
Uhusiano kati ya Tanzania na Rwanda kwa sasa unaonekana kulegalega kutokana na kitendo chake kupeleka majeshi yake kuungana na vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Mataifa (UN) vilivyoko Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) katika Jimbo la Goma.
Chanzo cha Uhasama
Uhasama huo unatokana na Kundi la M23 linaloundwa na wapiganaji wa Kitutsi likiaminika kusaidiwa na Rwanda na linapambana na majeshi ya Serikali ya DR Congo. Hata hivyo, Rwanda inapinga kuisaidia M23.
Kumekuwa na malumbano kupitia vyombo vya habari vya nchi hizo mbili huku kila upande ukirusha vijembe vya kumponda mwenzake.
Mbali na vijembe, hivi karibuni Rwanda imejitoa na kuanza kuacha kutumia Bandari ya Dar es Salaam kuingizia mizigo yake, badala yake sasa imejielekeza Mombasa nchini Kenya.
Hali hiyo inaonyesha kuiathiri Tanzania hata katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ambapo katika mikutano ya hivi karibuni ya wakuu wa nchi hizo, Rais Kikwete hakushiriki.
Mkutano huo uliofanyika wiki iliyopita mjini Mombasa na kuhudhuriwa na marais, Uhuru Kenyatta wa Kenya, Yoweri Museveni wa Uganda, Paul Kagame wa Rwanda, Pierre Nkurunzinza wa Burundi na Salva Kiir wa Sudan Kusini walialikwa na kutuma wajumbe wao, lakini bila kumhusisha Rais Kikwete ni moja ya dalili ya Tanzania kutengwa au kuenguliwa.
Baada ya mkutano huo, marais hao wamezindua eneo jipya la bandari ambalo litasaidia kuimarisha huduma ya kupakia na kupakua mizigo.
Serikali ya Kenya imesema ujenzi wa sehemu hiyo mpya umefanyika kwa kutumia kipato cha ndani bila msaada wowote kutoka nje.
Mkutano huo unafuatia ule wa mwezi Juni uliofanyika mjini Kampala, Uganda ambao pia Rais Kikwete hakualikwa.
Katika mkutano huo ilikubaliwa kwamba, nchi za Afrika Mashariki zipunguze gharama za usafirishaji bidhaa kwa kupanua usafiri wa reli pamoja na kuboresha huduma za bandari, hususan ile ya Mombasa sambamba na kuharakishwa ujenzi wa bandari kubwa visiwani Lamu.
Kutokana na hali hiyo, Tanzania sasa imemwomba Rais Museveni wa Uganda kuisuluhisha na Rwanda.
Akijibu swali la kingozi wa kambi rasmi ya upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, Waziri Mkuu Mizengo Pinda alisema:
“Rais Kikwete amemwomba Rais wa Uganda, Yoweri Museveni ili kuona jinsi ya kusuluhisha suala hili.”
Pamoja na usuluhishi huo wa Museveni, kiongozi aliyeingia madarakani mwaka 1985 na kuwa mmoja kati ya viongozi wa muda mrefu barani Afrika na katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, lakini hatima ya Tanzania kwenye EAC iko shakani.
Ni dalili mbaya
Akizungumzia suala hilo, Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Profesa Gaudence Mpangala anasema hiyo siyo dalili njema kwa uchumi wa Tanzania.
“Hiyo siyo dalili nzuri kabisa, mgogoro ulianza kati ya Rais Paul Kagame na Rais Kikwete, lakini sasa unaonekana kusambaa Jumuiya yote ya Afrika Mashariki. Kama wanafikia hadi kufanya mikutano bila kuishirikisha Tanzania, basi tutaathirika kiuchumi,” anasema Profesa Mpangala na kuongeza:
“Lengo la ushirikiano katika Jumuiya ya Afrika Mashariki kwanza ni uchumi na baadaye masuala ya siasa. Sasa ikitokea nchi inatengwa, ujue hali siyo nzuri.”
Kwa upande mwingine, Profesa Mpangala anazungumzia mchezo mchafu unaofanywa na Rwanda dhidi ya Tanzania ambaye ni mwenyeji katika jumuiya hiyo.
“Taratibu za kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki, sharti nchi iwe imejidhatiti kiusalama na amani. Sasa nchi za Rwanda na Burundi hazikuwa na sifa hiyo, lakini ziliingizwa tu. Matokeo yake sasa zinataka kuvuruga uhusiano na nchi wenyeji yaani Tanzania, Kenya na Uganda,” anasema.
Naye mhadhiri katika Chuo cha Ushirikiano wa Kimataifa na Diplomasia, Dk Kitojo Wetegire anasema mgogoro huo utavuruga malengo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
“Ushirikiano wowote unapohusisha mataifa au makundi mbalimbali, lazima kuwepo na makubaliano maalumu ya kuulinda. Afrika Mashariki tumeungana ili kuinua uchumi wetu, uzalishaji na masoko. Sasa malengo hayo hayatafikiwa kama kunakuwa na migogoro yote hii,” anasema Dk Wetegire.
Nini kifanyike?
Wakati tayari Tanzania imeshamwomba Rais Museveni kusuluhisha mgogoro huo, wasomi hawa wanaunga mkono usuluhishi huo japo kwa wasiwasi.
Profesa Mpangala anatilia wasiwasi usuluhishi wa Rais Museveni akirejea historia ya Wahima (Hima empire) inayowahusisha makabila ya Watutsi na Ankole.
“Siyo mbaya kwa Museveni kutusuluhisha, lakini ni rafiki mkubwa wa Kagame. Wameshirikiana kwenye vita nyingi; kwa mfano Kagame alimsaidia Museveni katika mapambano ya kuingia madarakani na Museveni alimsaidia mwenzake wakati wa kuingia madarakani mwaka 1994, sasa kwa hali hiyo… sijui,” anasema Profesa Mpangala na kuongeza:
“Kulikuwa na uvumi wa Hima empire ambapo inadaiwa kuwa Museveni na Kagame wana mkakati wa kuirudisha Afrika Mashariki kwenye tawala za kizamani ambapo Wahima walitawala eneo kubwa. Japo Museveni mwenyewe amekuwa akikanusha, lakini wanaweza kuiteka Kenya, Uganda, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.”
Nini kifanyike
Kwa upande wake Dk Kitojo anasema suluhisho ni Rwanda na Tanzania kukaa meza moja na kusuluhishwa.
“Suluhisho hapa ni Rwanda na Tanzania kukaa mezani na kusuluhishwa. Tatizo kila nchi inajifanya kuwa na ubabe na wamekalia kulumbana tu kwenye vyombo vya habari. Ni kweli Tanzania ina ushawishi mkubwa wa kimataifa, lakini hiyo haitasaidia kitu,” anasema Dk Kitojo.
Ameunga mkono kauli ya Rais Kikwete ya kuitaka Serikali ya Rwanda ipatane na FDLR na kitendo cha kupelekwa kwa wanajeshi wa Tanzania kulinda amani Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
“Hoja ya Rais wa Marekani, Barack Obama kuitembelea Tanzania kwamba ndiyo iwe chanzo cha kutengwa kwa Tanzania kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki haina nguvu. Kikubwa hapo ni ushauri wa Rais Kikwete kwa Serikali ya Rwanda kupatana na FDLR, jambo ambalo ni sahihi,” anasema na kuongeza:
“Uhasama mwingine ni Tanzania kupeleka jeshi la kulinda amani Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Kama Rwanda haikufurahishwa basi ina maslahi binafsi.
Source: Mwananchi