Home » Unlabelled » Diamond aitawala ‘front page’ ya Mtanzania leo, utajiri wake wahusishwa na biashara ya unga
Diamond aitawala ‘front page’ ya Mtanzania leo, utajiri wake wahusishwa na biashara ya unga
Kwa mara ya kwanza Diamond Platnumz leo ameitawala front page ya
gazeti la kila siku la Mtanzania kwa habari yenye kichwa ‘Diamond atajwa sakata la ‘unga’.
Gazeti la Mtanzania limeandika:
KWA mara ya kwanza tangu lilipoibuka sakata la watu maarufu kujihusisha ama na utumiaji au usafirishaji wa dawa za kulevya, jina la mwanamuziki anayeaminika kuwa na ukwasi mkubwa kwa sasa hapa nchini, Nasseeb Abdulmaliki, maarufu zaidi kwa jina la Diamond, limeanza kutajwa kuwa ni miongoni mwa vigogo wa ‘unga.’
Tayari mjadala mkubwa wa chini chini umeibuka kwa watu
mbalimbali wakiwemo mashabiki wake, na taarifa ambazo zimelifikia MTANZANIA
Jumatano kutoka vyanzo mbalimbali zimedai kuwa, mwenendo wa maisha ya Diamond
sasa unachunguzwa na baadhi ya maofisa wa vyombo vya dola vya ulinzi na
usalama.
Kutajwa kwa jina la Diamond katika sakata hili, kunatiwa nguvu
zaidi na mwenendo binafsi wa maisha wa msanii huyo maarufu wa muziki wa kizazi
kipya, unaokwenda sambamba na ukwasi mkubwa alioupata katika kipindi kifupi.
Kama hiyo haitoshi, safari za nje ya nchi za mwanamuziki huyo
unaohusisha ziara zake nchini Afrika Kusini na Uingereza, pia ni mambo ambayo
yamechochea wingu la mashaka lililofikia hatua ya jina lake kuingizwa katika
mtandao huo ambao katika siku za karibuni, umewagusa pia baadhi ya watu wenye
majina makubwa katika jamii.
Kuhusu ziara hizo, kilicholeta mshtuko na dukuduku dhidi yake ni
kuwapo kwa taarifa kwamba, katika moja ya ziara hizo za nje ya nchi, Diamond
alifikia hatua ya kusafiri akitumia chumba kinachotumiwa na wageni mashuhuri
(VIP), badala ya njia ya wasafiri wa kawaida.
Mbali na hilo, taarifa nyingine zinaeleza kwamba, mizigo ya
msanii huyo ambaye mara kadhaa amekuwa akisafiri na kundi la wacheza shoo wake,
imekuwa ikipita pasipo kupitishwa katika hatua za ukaguzi kwa namna ile ile
ilivyokuwa kwa mabinti wawili wa Kitanzania walionaswa nchini Afrika Kusini
baada ya kuruka mfumo wa ukaguzi wa JNIA.
Aidha, ukaribu wa kimahusiano kati ya Diamond na baadhi ya
Watanzania wanaoishi nchini Afrika Kusini na ambao majina yao pia yameanza
kuhusishwa na biashara hiyo ya mihadarati, ni jambo jingine ambalo limechochea
harakati za kufuatiliwa kwa karibu kwa nyendo za Diamond.
Taarifa zaidi kutoka JNIA zinaeleza kwamba, miongoni mwa watu
wanaoweza wakawa wamemponza Diamond ni wale ambao walionekana kuwa karibu na
Agness Gerald ‘Masogange’ (25) na Melisa Edward (24), siku walipokuwa
wakisafiri kwenda Afrika Kusini kabla hawajanaswa katika uwanja wa Ndege wa Oliver
Thambo jijini Johannesburg nchini Afrika Kusini, wakiwa na shehena ya dawa za
kulevya.
Mwenendo wa watu hao unatiliwa shaka kuwa huenda ni miongoni mwa
wafanyabiashara wakubwa wa dawa za kulevya wenye maskani yao nchini Afrika
Kusini, kwa sababu mbali na ukaribu na wasichana hao, pia walihusika kwa karibu
kuusafirisha mwili wa mwanamuziki Albert Mangwair, aliyefia huko huko Afrika
Kusini ambaye taarifa za kufa kwake ziligumbikwa na matumizi ya dawa za
kulevya.
Alipoulizwa jana na MTANZANIA Jumatano kupitia simu yake ya
kiganjani kuhusu taarifa hizo na iwapo amekwishahojiwa na vyombo vya dola baada
ya jina lake kuanza kutajwa kuwa miongoni mwa orodha ya wasanii wa muziki
wanaosafirisha dawa za kulevya, Diamond alikiri kuwa na pesa za kutosha kuishi
maisha anayoyataka, lakini akakana kujihusisha na biashara hiyo.
Akifafanua tuhuma moja baada ya nyingine kwa mpangilio aliokuwa
akiulizwa na gazeti hili, Diamond alisema katika maisha yake, hajawahi
kujihusisha na utumiaji au usafirishaji dawa za kulevya, lakini madai hayo
yamekuwa yakitolewa dhidi yake na watu ambao hawajui siri ya mafanikio yake.
“Kazi ngumu siku zote inalipa, sasa napata matunda ambayo
yanatokana na kile nilichokifanya, iweje watu wanitilie mashaka, Watanzania ni
mashahidi wangu wananiona navyochumia juani, nitaendelea kulia kivulini tu
kwani nakula kwa jasho langu.
“Siyo kweli kwamba mizigo yangu haikukaguliwa na kama
haikukaguliwa na ingekuwa na kasoro, basi Uingereza wangenitia hatiani,
nilipita na nilikaguliwa.” Alisema Diamond.
Alipoulizwa kuhusu taarifa za kuwa mwanamtandao wa kundi la
Masogange, pia alikanusha kwa kueleza kuwa hata siku aliyosafiri kwenda Afrika
Kusini alikwenda peke yake uwanja wa ndege na kuongeza kuwa alikwenda huko kwa
shughuli za kimuziki, ambapo safari nzima iligharimu zaidi ya Dola 30,000 za
Kimarekani.
“Afrika Kusini nimekwenda kufanya kazi zangu na safari hiyo
imenigharimu zaidi ya Dola 30,000, nilikwenda kurekodi nyimbo yangu mpya
inayoitwa namba moja ambayo itaanza kusikika hivi karibuni.
“Unajua Watanzania sasa hivi wanajua mtu hawezi kufanikiwa au
kupata maendeleo bila kuuza ‘unga’, hili si sawa juhudi za mtu ndizo
zinamfikisha alipo, na mimi juhudi zangu ndio zinanifikisha hapa, watu waache
kunijadili vibaya.” Alisema Diamond.
Kuibuka kwa taarifa hizi kumekuja ikiwa ni takribani miezi
miwili sasa tangu Watanzania wawili, Agness Gerald ‘Masogange’ (25) na Melisa
Edward (24), waliokuwa na uhusiano wa karibu na baadhi ya wanamuziki maarufu
hapa nchini, kukamatwa nchini Afrika Kusini wakiwa na dawa za kulevya aina ya
Crystal Methamphetamine zenye thamani ya Sh bilioni 6.8.
Mbali na kuwa na uhusiano wa karibu na wanamuziki, Edward
anadaiwa kuwa alikuwa mfanyakazi katika mgahawa mmoja maarufu jijini Dar es
Salaam, unaomilikiwa na mmoja wa vijana matajiri hapa nchini ambaye hata hivyo
gazeti hili halijafanikiwa kumpata ili kufanya naye mahojiano.
Wakati huo huo, tayari hatua za kinidhamu zimekwishaanza
kuchukuliwa dhidi ya wafanyakazi wa JNIA waliohusika kupitisha kilo 150 za dawa
za kulevya, ambao Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, ametaja majina
yao hivi karibuni na kuonyesha kwa waandishi wa habari ushahidi wa kuhusika
kwao.
You may also Like
Followers
Tags 2
Popular Posts
-
New AUDIO | Geez Mabovu - Story | Download Sikiliza & Download Nyimbo ya Marehemu GEEZ MABOVU akiwa amemshirikisha GALATONE