Aina Mbili Ya Vyakula Hutakiwi Kuvila Baada Ya Mazoezi



KAMA wewe ni miongoni mwa watu wenye utaratibu wa kufanya mazoezi ya mwili kila siku au mara kwa mara unahitaji kusoma makala haya kwa makini, kwani yanahusu suala muhimu ambalo pengine hukuwahi kulijua kabla.
Inaeleweka na kukubalika na tafiti zote kuwa mazoezi ya mwili ni miongoni mwa vitu muhimu kiafya kufanywa na mtu 
baada ya kuzingatia lishe. Imeelezwa pia kwamba mazoezi yanachukua asilimia 20 ya ustawi wa afya ya mtu, hii ina maana kwamba hata kama utakula vyakula sahihi, kama hufanyi mazoezi, ubora wa afya yako utakuwa haujakamilika kwa asilimia 20.

Aidha, unajua kwamba chakula chochote unachokula mara baada ya kufanya mazoezi ndani ya muda wa masaa 2, una athari kubwa katika faida unazoweza kuzipata kutokana na mazoezi unayoyafanya? Elewa kwamba unachokula muda huo kinaweza kuijenga au kuibomoa afya yako, licha ya mazoezi unayoyafanya.

SUKARI
Kuna aina mbili ya vyakula au vitu ambavyo hutakiwi kuvila mara baada ya kumaliza kufanya mazoezi, moja ya vyakula hivyo ni sukari tunayoitumia kwenye matumizi yetu ya kila siku katika vinywaji na vyakula tunavyokula majumbani.
Imeeleezwa kuwa utumiaji wa sukari ndani ya muda wa masaa mawili mara baada ya kumaliza kufanya mazoezi, huvuruga mfumo wa homoni za ukuaji wa mwili na mfumo wa urekebishaji wa kiwango cha sukari mwilini, ambacho kinaweza kusababisha ugonjwa wa kisukari.
Utafiti wa hivi karibuni wa jarida la Applied Physiology la nchini Marekani umegundua kwamba badala ya kula sukari au vyakula na vinywaji vyenye sukari, inashauriwa kula vyakula vyenye kiwango kidogo cha wanga ambavyo huepusha magonjwa ya kisukari (Type2) na magonjwa mengine ya moyo. Vyakula hivyo ni pamoja na viazi, mkate, muhogo, karanga au korosho n.k.

FRUCTOSE
‘Fructose’ ni jamii ya sukari ambayo hutumika zaidi kwenye vinywaji kama juisi na vinywaji vingine vya baridi, zikiwemo soda. Aina zote za vinywaji vyenye sukari aina hii vinapotumiwa muda mfupi baada ya mazoezi, navyo huharibu mfumo wa homoni za ukuaji wa mwili na husababisha ugonjwa wa kisukari.
Mbali ya kupata athari hizo kama zilivyotajwa hapo juu, vilevile utakosa faida za mazoezi za kupunguza mafuta mwilini, badala yake utajikuta unafanya mazoezi ya mwili, badala ya kupungua ukajikuta unaongezeka uzito au unabaki na uzito huohuo kila siku.
Suala la kujiepusha na unywaji wa vinywaji vyenye sukari nyingi ni muhimu sana iwapo unafanya mazoezi kwa minajili ya kupunguza mafuta mwilini na kupunguza uzito. Vinywaji hivyo ni pamoja na vile vinavyojulikana kwa majina ya ‘Energy Drink’ ambavyo mara nyingi huwa na sukari nyingi.
Mwisho, jitahidi kunywa maji ya kutosha mara baada ya kupumzika, hasa kama mazoezi unayoyafanya yanasababisha kutokwa na jasho jingi ambalo hutoka ili kuondoa sumu lakini hupunguza maji mwilini.

Recent Posts