Anayetuhumiwa kumuua Padri Mushi akamatwa

Jeshi la Polisi limemkamata na linamshikilia mtu anayedaiwa kumpiga risasi na kumuua, Padri Evarist Mushi wa Kanisa Katoliki Zanzibar mwezi uliopita.

Jeshi hilo limesema kuwa tayari jalada la mtu huyo limekwishapelekwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) Zanzibar kwa hatua za kufikishwa mahakamani.
Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa aliwaambia waandishi wa habari jana mjini hapa kuwa mtu huyo ni Omar Mussa Makame anayeishi Mtaa wa Raha Leo mjini hapa.
Jeshi la Polisi Zanzibar lilishirikiana na Askari wa Upelelezi wa Marekani (FBI) waliotoka Nairobi, Kenya kumsaka mtu huyo anayedaiwa kumpiga risasi padri huyo wakati akienda kuongoza ibada ya Jumapili katika Kanisa la Mtakatifu Teresia lililopo Beit el Raas, nje kidogo ya mji, Februari 17 mwaka huu.
“Najua si nyinyi tu waandishi wa habari lakini Watanzania wote wanataka kujua maendeleo ya upelelezi wa kuuawa Padri Evarist Mushi.
Jeshi la Polisi liliwaahidi litawajulisha kila hatua iliyofikiwa juu ya upelelezi wa shauri hili,” Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa aliwaambiwa waandishi wa habari jana.
“Mpaka hapa tunapozungumza upelelezi wa shauri hili umefikia hatua nzuri na jalada la shauri hili limeshapelekwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka kwa hatua za kisheria.
Mhusika wa mauaji haya tayari amekamatwa na ametambuliwa na watu walioshuhudia tukio hilo,” alisema kamishna huyo.
“Jeshi la Polisi mbali na hatua kadhaa za kiupelelezi walizozichukua ilikuwa ni pamoja na kuchora michoro ya sura ya mtu kwa kutumia watu walioshuhudia tukio hilo.
Baada ya kuitoa picha hiyo katika vyombo mbalimbali vya kiulinzi, wananchi, vyombo vya habari na mitandao ya kijamii mhalifu huyo ametambulika na kutambuliwa,” alisema Kamishna Mussa.
Alisema kuwa Jeshi la Polisi liliahidi kutoa zawadi ya Sh10 milioni kwa mtu atayewezesha kupatikana kwa muuaji huyo na shahidi aliyemtaja mtu huyo atapewa kiasi hicho cha fedha lakini kwa usalama hatatangazwa.
Kuuawa kwa Padri Mushi ni tukio la tatu kubwa la kushambuliwa viongozi wa dini Zanzibar baada ya kumwagiwa tindikali Katibu wa Mufti, Fadhil Soraga na kupigwa risasi Padri Ambrose Mkenda wa Kanisa Katoliki.
Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi Zanzibar limeweka ulinzi mkali katika nyumba za ibada wakati wa sherehe za Pasaka ili kuhakikisha kunakuwa na usalama.
Mbali na kuweka ulinzi kwenye nyumba za ibada za dini zote, pia Polisi imeimarisha ulinzi mitaani na katika nyumba za starehe.
 “Jeshi la Polisi litaendelea kufanya doria zikiwemo za magari, miguu, pikipiki na mbwa katika maeneo mbalimbali ya miji na vijiji kuanzia leo (jana) mpaka baada ya mapumziko ya Pasaka,” taarifa iliyotolewa na Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa ilisema.
Wanamichezo wapatao 4,000 wameingia Zanzibar kutoka Tanzania Bara kwa ajili ya tamasha la michezo linalofanyika kwa zamu baina ya sehemu hizo mbili wakati wa mapumziko ya Pasaka.
Kamishna Mussa aliwataka wananchi na wageni wasiwe na hofu na kwamba washirikiane na jeshi lake katika kuhakikisha usalama unadumu.
Vimekuwapo vitisho kwa siku kadhaa kwamba yatatokea machafuko wakati wa kipindi hiki cha sherehe za Pasaka.

0 comments:

Post a Comment

Recent Posts