MAMBO YATAKAYOKUSAIDIA KUBADILISHA MAISHA YAKO MWAKA 2014
Mwaka mpya na mambo mapya, unapoupokea mwaka 2014 ni vyema ukafurahia mafanikio uliyopata mwaka uliopita. Hata kama mafanikio hayo ni kiduchu bado unayosababu ya kujisifu na kujipongeza kwakuwa umekuwa mtendaji wa mambo yako na kufanikiwa. Kujipongeza na kufurahia mavuno yako ya mwaka uliopita ni muhimu sana kwakuwa ni chachu ya wewe kuona kuwa unaweza fanya mambo makubwa zaidi ikiwa utajipanga vyema na kukusudia kufanikiwa katika mambo utakayokuwa na mipango nayo kwa mwaka 2014.
Pia kwakuwa katika kila mafanikio hapakosi kuwa na changamoto, ni vyema ukajifunza kutokana na chagamoto zote ulizopata kwa mwaka 2013, ukatambua kasoro ulizoziona na mapungufu uliyonayo kwa lengo la kujiimarisha ili mwaka 2014 uwe bora na wenye mafanikio makubwa kwako.
Soma hapo chini mambo yatakayokusaidia kubadilisha maisha yako mwaka 2014 ili kupata matokeo mazuri zaidi na yenye tija kwa maisha yako.
1. Kuwa na fikra pana kwa kukubali kubadilisha maisha yako.
Wewe si mtu tena kama wa mwaka uliopita. Unaweza kuwa ulifanya mambo mengi ambayo ni mazuri sana labda hata yakuweza kuigwa lakini kwa upande mwingine kuna mapungufu uliyaona kwako kwa mwaka 2013. Ni mapungufu haya ndiyo unayopaswa kujirekebisha. Watu hubadilika kwa namna moja au nyingine, katika maisha mambo hubadilika kila wakati. Mambo hayo ndiyo maisha. Kuna vitu vingine hutamani kabisa viendelee kuwepo katika maisha yako, na hapa ndipo panapohitaji uamuzi sahihi wa wewe kuondokana na yale yote ambayo kuyataki.
Tafakari kuhusu maisha kwa nia ya kutaka kukua na kubadilisha maisha yako. Hapa huwa ndipo pagumu kwasababu swala la kubadilika humfanya mtu aumie. Nasema hivyo kwasababu mtu kuachana na mambo anayoyapenda japo hayana faida kwake ni swala gumu sana.
Mfano: Mtu kujizuia kunywa pombe kupita kiasi, mtu kuachana na tabia ya umbea kufuatilia yasiyomhusu, mtu kuachana na kula vyakula vyenye madhara kwa afya yake kama ulaji wa vyakula vyenye sukari nyingi au mafuta mengi nakadhalika. Maumivu ya kubadilika ni bora kuliko maumivu ya kujutia. Maumivu ya kujutia ni yale ambayo hapo baadae utajilaumu kufanya makosa kwanini hukuamua kuachana na mambo mabaya. Unaweza kujutia kwanini hukuamua kubadilika na kufanya mambo makubwa uliyoazimia kufanikisha ambayo huenda yangekufanya ufurahie maisha yako kwa sasa. Ukweli ni kwamba huwezi kukua na kufanya mambo makubwa ikiwa utaendelea kuyashikilia makosa uliyofanya mwaka uliopita, mwezi uliopita au siku iliyopita. Usijutie sana makosa uliyofanya mwaka 2013 kwasababu maisha siku zote hutoa nafasi ya pili ya kuweka mambo sawa. Nafasi hiyo ya pili huitwa ''KESHO'' hivyo unayo nafasi ya kujirekebisha na kufanya mambo mengi mazuri mwaka 2014.
2. Amua huu ndio wakati muafaka wa kufanya mambo ya msingi katika maisha yako.
Tambua ni mambo gani ya msingi unayotaka kufanikiwa katika maisha yako, weka pembeni mambo yote ambayo si muhimu kwako. Huu sio wakati wa kupoteza tena bali ni wakati wa kufanikiwa na kupata utakayo, yawekee kipaumbele mambo ambayo ni ya msingi kwako kisha jipange na kuwa mtendaji katika kuendea mipango yako. Katika mipango hiyo usisahau kuweka mambo muhimu mbele, pia usichanganye mambo muhimu na yale yasiyo na manufaa katika maisha yako.
3. Kubali mapungufu yako ili ukue.
Unaweza usiwe mahali unapopataka kwa sasa ila kwakuwa una malengo na nia thabiti ya kufanikiwa bila shaka utafika. Una sababu nzuri ya kufikiri UNAWEZA kutimiza malengo yako au ndoto kubwa uliyonayo. Sio tu kwasababu umefanya chaguo sahihi bali ni kwakuwa tayari umeshashinda yale mabaya kwa kupiga hatua ndogo ya kukubali mabadiliko katika maisha yako na kuelekea katika njia sahihi.
Bila kujali mapungufu yako, fanya mambo sahihi kwa kadri uwezavyo. Usijali udhaifu ulionao iwe ni uwoga, ulemavu wa kiungo cha mwili au kasoro yeyote ile uliyonayo. Ukiondoa wasiwasi kila jambo jema lilokusudiwa kuwa zawadi kwako litakufuata na mambo yote mabaya yatapotea hivyo huna sababu ya kuwa na hofu.
4. Amua kubadilika kwa kusema yaliyopita yanatosha.
Jiambie mwenyewe yaliyopita ‘’YANATOSHA’’ na kubali makosa yako. Usiyafiche mapungufu yako na kamwe usijidanganye. Linapokuja swala la msingi kuhusu maisha yako usiwe mjinga kwa kujidanganya kwa namna yeyote ile. Jikubali na jifunze kutokana na yale yote yaliyotokea katika maisha yako. Wewe ni WEWE na una kila sababu ya kufanya mambo makubwa unayotamani kufanikiwa. Sikiliza moyo wako na fuata vile hisia zako zinavyokuambia. Usiogope kufanya kile kitu unachopenda kwakuwa ni uamuzi wako, furahia kuwa WEWE na usikubali kubadilisha mawazo yako kwasababu ya mtu mwingine kutokukuelewa au kutokubali maamuzi yako. Usikubali mtu mwingine akupotoshe kwa kile unachoamini ni ukweli, ishi maisha yako kwa namna unavyoona ni sahihi na furahia maisha.
5. Kuwa na mahusiano sahihi.
Sio kila mtu atakusifu au kukukubali kwa kile unachofanya, ni vyema ukawatambua rafiki na jamaa zako wa kweli na wale ambao ni wakaidi kwako. Ikiwa nguvu zako na muda wako utatumika katika mahusiano mabaya au katika kufanya shughuli nyingi na kulazimika kupuuza uhusiano wako na watu wengine ambao ni muhimu kwako ni wazi kuwa utaishia pabaya. Ni vizuri kujipenda mwenyewe bila kusahau kuonyesha upendo wako kwa wengine unaowajali. Chagua kuwa na watu sahihi ambao wapo nawe katika kila hali na hakika kwa namna moja au nyingine watachangia katika maendeleo ya maisha yako.
6. Ongeza upeo wako wa elimu.
Ishi kwa kupenda kujisomea, utajifunza mengi sana ya ulimwenguni. Unapojifunza na kujua mambo mengi mazuri ndivyo nawe utakavyoishi maisha mazuri zaidi. Kusoma kunaweza kuwa si yale mambo ya darasani tu bali mambo yoyote yale yanayokujenga kiroho, kiakili, kimwili na maisha yako kwa ujumla.
Unaweza soma pia: Faida saba (7) za kupenda kujisomea.
7. Chukua nafasi ya kufuata ndoto zako.
Kila mtu ana ndoto, lakini matumaini ya ndoto hizo sio sawa kwa kila mtu. Usiwe wale watu wenye ndoto ndogo au wenye mawazo mafupi. Linapokuja swala kuhusu WEWE siku zote kuwa na malengo makubwa ikiwezekana ndoto hiyo iwashangaze watu. Na raha huja pale ambapo watu walisema hutoweza na ukadhihirisha kuwa imewezekana. Mtu mwenye ndoto kubwa huwa juu siku zote na hawezi kufananishwa na mtu mdogo hata kidogo. CHAGUA KUWA MTU MKUBWA.
Kwa hayo mambo machache naamini yatakusaidia kuweza kubadilisha maisha yako kwa mwaka 2014. Kikubwa jiamini, jiwekee malengo na uwe mtendaji wa mipango yako hakika mafanikio yapo mbele yanakungojea.
- See more at: http://kamotta.blogspot.com/#sthash.Y7S6D4od.dpuf
0 comments: