ICC:Afueni kwa Kenyatta japo kwa masharti
Kenyatta katika mahakama ya ICC |
Hii inafuatia ombi la Rais Kenyatta kutaka kuruhusiwa kutohudhuria vikao vya kesi dhidi yake kutokana na majukumu yake kama Rais wa Kenya.
Hata hivyo Kenyatta ametakiwa kuwepo mahakamani kwa ufunguzi wote wa kesi dhidi yake, hotuba za ufunguzi wa pande zote husika , kusikiliza maoni ya waathiriwa na wasiwasi wao , uamuzi utakapotolewa na vikao vyovyote atakavyotakiwa na majaji kuhudhuria.
Ikiwa itawezekana Kenyatta pia atatakiwa kuhudhuria kikao cha uamuzi wa kesi yake.
Iliamuliwa kuwa ikiwa Rais Kenyatta atakosa kutii masharti hayo , basi huenda majaji nao wakamuondolea faida hizo na kutolewa kwa kibali cha kumkamata.
Naibu Rais Ruto pia amepata afueni hiyo ila kwa masharti yaliyotolewa kwa Kenyatta ili kuwawezesha kuendelea na majukumu yao kama viongozi wa nchi.
Majaji pia wamesema wameamua kutoa masharti haya kwa Kenyatta ili kutoonekana kuwa na mapendeleo dhidi ya Kenyatta na kuonyesha heshima kwa haki za mshukiwa lakini pia kuwalinda waathiriwa na mashahidi katika kesi hiyo.
Rais Kenyatta amekuwa akiitaka mahakama ya ICC kumruhusu kutohudhuria kesi yake kutokana na majukumu yake kama Rais wa Kenya.
Ombi hili liliwasilishwa kupitia kwa Muungano wa Afrika ambao ulisema kuwa utawasilisha malalamiko yake kwa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kuwa mahakama ICC inatumika kuwakandamiza viongozi wa Afrika.
Muungano huo ulimshauri Kenyatta na naibu wake kutohudhuria kesi zao kwani wao ni viongozi wa nchi na wanapaswa kuruhusiwa kuendelea na majukumu yao kama viongozi wa Kenya.
Cha zaidi AU ilitaka kesi dhidi ya Kenyatta kuahirishwa kwa mwaka mmoja. Kenyatta na Ruto wanatuhumiwa kwa kuongoza ghasia za kikabila zilizozuka baada ya uchaguzi mkuu mwaka 2007/2008 ambapo zaidi ya watu elfu moja walifariki.
0 comments: