KAROTI KINGA DHIDI YA SARATANI NA UGONJWA WA MOYO
Kwa ujumla wake, karoti ni mboga yenye kiasi kingi cha Vitamin
A. Mbali ya vitamini hiyo, karoti ina virutubisho vingine muhimu vyenye uwezo
wa kuzuia magonjwa hatari, kama vile saratani, moyo na mengine mengi na kumbuka
kwamba; ‘kinga ni bora kuliko tiba’.
Sifa pekee na kubwa kuhusu karoti inayojulikana na watu wengi, ni uwezo wake wa
kuimarisha nuru ya macho na uwezo wa kuona, hususan wakati wa usiku. Katika
makala ya leo nitakufahamisha faida nyingine za mboga hii rahisi, inayopatikana
kwa wingi, mijini na vijijini. Ukiielewa vizuri, itaokoa maisha yako.
VIRUTUBISHO VYA KAROTI
Kwa mujibu wa tafiti kadhaa zilizofanywa, imethibitika kuwa karoti ina kiwango
kikubwa cha virutubisho jamii ya ‘carotenoids’ ambavyo husaidia sana kuupa
mwili uwezo wake wa asili wa kupambana na maradhi yanayojitokeza mwilini.
Katika utafiti huo, imeelezwa kuwa ulaji wa karoti, hata kwa kiasi cha karoti
moja tu kwa siku, kinampunguzia mlaji uwezekano wa kupatwa na ugonjwa wa
saratani ya matiti kwa asilimia 20.
Aidha, imeainishwa zaidi kuwa, mlaji wa karoti moja kwa siku, atakuwa pia
anajiepusha na kupatwa na saratani za aina nyingine kwa asilimia 50. Saratani
hizo zimetajwa kuwa ni saratani ya kibofu cha mkojo, kizazi, utumbo, mapafu na
saratani ya koo.
Katika utafiti wa hivi karibuni wa Taasisi ya Saratani ya Taifa nchini Marekani
(National Cancer Institute), imebainika kuwa wagonjwa wengi waliogundulika na
saratani ya mapafu, katika milo yao walikuwa hawatumii karoti wala vyakula
vingine vyenye virutubisho jamii ya ‘carotenoids’.
KAROTI NA UGONJWA WA KISUKARI
Kama tujuavyo, ugonjwa wa sukari ni maradhi yanayowasumbua watu wengi duniani
na hauna tiba. Magonjwa kama kisukari, huweza kumpata mtu kutokana na mpangilio
mbaya wa vyakula anavyokula kila siku na staili ya maisha anayoishi kwa ujumla.
Mtu anaweza kujiepusha na magonjwa mengi hatari, kama kisukari, kwa kuzingatia
ulaji usahihi. Kutokana na kiwango cha virutubisho mbalimbali vilivyomo kwenye
karoti, mgonjwa wa kisukari anaweza kupata ahueni kwa kufanya karoti kuwa
sehemu ya mlo wake wa kila siku.
Watafiti wamegundua kwamba virutubisho vilivyomo kwenye karoti, vina uwezo
mkubwa wa kurekebisha kiwango cha sukari mwilini, hivyo kutoa kinga au kumpa
mgonjwa nafuu kubwa.
KAROTI NA MAPAFU
Kama unaishi au unafanyakazi katika mazingira yenye moshi au wewe ni mvutaji wa
sigara, ulaji wa vyakula vyenye vitamin A kwa wingi kama karoti, humuepusha
mvutaji na uwezekano wa kupatwa na saratani ya mapafu. Ulaji wa vyakula aina
hii kwa mvuta sigara, si wa hiyari kama anataka kujiepusha na saratani ya
mapafu.
JINSI YA KUCHAGUA NA KUHIFADHI KAROTI
Kwa kawaida, karoti huwa ni mzizi ulionyooka wenye rangi za kung’aa. Zipo
karoti za rangi tofauti, lakini karoti bora ni ile tuliyoizoea yenye rangi ya
chungwa na kwa mujibu wa utafiti, karoti yenye rangi iliyoiva sana ndiyo yenye
virubisho vingi zaidi.
Karoti inaweza kudumu kwa muda mrefu ikihifadhiwa vizuri. Hifadhi karoti yako
kwenye jokofu ikiwa kwenye mfuko wa plastiki ambao hauruhusu kupitisha hewa
nyingine, ikihifadhiwa vyema, karoti inaweza kukaa hadi wiki mbili bila
kuharibika.
Aidha, wakati wa kuhifadhi karoti yako katika jokofu, usichanganye na matunda
mengine kama vile ‘peasi’, nyanya, ‘epo’ na matunda mengine ya jamii hiyo.
Inaelezwa kuwa kwa matunda hayo kukaa pamoja, kunaweza kuifanya karoti kuwa
chungu.
Kabla ya kuhifadhi karoti kwenye jokofu, hakikisha umekata majani yake ya juu
na mizizi yake ya chini, ili kuzuia karoti kuchipua licha ya kuwa kwenye
jokofu.
JINSI YA KUANDAA NA KUILA KAROTI
Osha vizuri karoti yako kwa kutumia kifaa maalumu cha kusugulia pamoja na maji
safi. Wakati wa kuosha karoti, vizuri utumie maji ya kutiririka na siyo
yaliyotuama. Hii inamaana kwamba osha karoti kwenye maji ya bomba au kwa
kumimina na chombo, usioshee ndani ya chombo kuepuka kuondoka na vijidudu.