Anayetuhumiwa kumuua Padri Mushi akamatwa
Jeshi la Polisi limemkamata na linamshikilia mtu anayedaiwa kumpiga risasi na kumuua, Padri Evarist Mushi wa Kanisa Katoliki Zanzibar mwezi uliopita.
Jeshi hilo limesema kuwa tayari jalada la mtu huyo
limekwishapelekwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) Zanzibar kwa hatua
za kufikishwa mahakamani.
Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa
aliwaambia waandishi wa habari jana mjini hapa kuwa mtu huyo ni Omar
Mussa Makame anayeishi Mtaa wa Raha Leo mjini hapa.
Jeshi la Polisi Zanzibar lilishirikiana na Askari
wa Upelelezi wa Marekani (FBI) waliotoka Nairobi, Kenya kumsaka mtu huyo
anayedaiwa kumpiga risasi padri huyo wakati akienda kuongoza ibada ya
Jumapili katika Kanisa la Mtakatifu Teresia lililopo Beit el Raas, nje
kidogo ya mji, Februari 17 mwaka huu.
“Najua si nyinyi tu waandishi wa habari lakini
Watanzania wote wanataka kujua maendeleo ya upelelezi wa kuuawa Padri
Evarist Mushi.
Jeshi la Polisi liliwaahidi litawajulisha kila
hatua iliyofikiwa juu ya upelelezi wa shauri hili,” Kamishna wa Polisi
Zanzibar, Mussa Ali Mussa aliwaambiwa waandishi wa habari jana.
“Mpaka hapa tunapozungumza upelelezi wa shauri
hili umefikia hatua nzuri na jalada la shauri hili limeshapelekwa kwa
Mkurugenzi wa Mashtaka kwa hatua za kisheria.
Mhusika wa mauaji haya tayari amekamatwa na ametambuliwa na watu walioshuhudia tukio hilo,” alisema kamishna huyo.
“Jeshi la Polisi mbali na hatua kadhaa za
kiupelelezi walizozichukua ilikuwa ni pamoja na kuchora michoro ya sura
ya mtu kwa kutumia watu walioshuhudia tukio hilo.
Baada ya kuitoa picha hiyo katika vyombo
mbalimbali vya kiulinzi, wananchi, vyombo vya habari na mitandao ya
kijamii mhalifu huyo ametambulika na kutambuliwa,” alisema Kamishna
Mussa.
Alisema kuwa Jeshi la Polisi liliahidi kutoa
zawadi ya Sh10 milioni kwa mtu atayewezesha kupatikana kwa muuaji huyo
na shahidi aliyemtaja mtu huyo atapewa kiasi hicho cha fedha lakini kwa
usalama hatatangazwa.
Kuuawa kwa Padri Mushi ni tukio la tatu kubwa la
kushambuliwa viongozi wa dini Zanzibar baada ya kumwagiwa tindikali
Katibu wa Mufti, Fadhil Soraga na kupigwa risasi Padri Ambrose Mkenda wa
Kanisa Katoliki.
Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi Zanzibar limeweka ulinzi
mkali katika nyumba za ibada wakati wa sherehe za Pasaka ili kuhakikisha
kunakuwa na usalama.
Mbali na kuweka ulinzi kwenye nyumba za ibada za dini zote, pia Polisi imeimarisha ulinzi mitaani na katika nyumba za starehe.
“Jeshi la Polisi litaendelea kufanya doria
zikiwemo za magari, miguu, pikipiki na mbwa katika maeneo mbalimbali ya
miji na vijiji kuanzia leo (jana) mpaka baada ya mapumziko ya Pasaka,”
taarifa iliyotolewa na Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa
ilisema.
Wanamichezo wapatao 4,000 wameingia Zanzibar
kutoka Tanzania Bara kwa ajili ya tamasha la michezo linalofanyika kwa
zamu baina ya sehemu hizo mbili wakati wa mapumziko ya Pasaka.
Kamishna Mussa aliwataka wananchi na wageni wasiwe
na hofu na kwamba washirikiane na jeshi lake katika kuhakikisha usalama
unadumu.
Vimekuwapo vitisho kwa siku kadhaa kwamba yatatokea machafuko wakati wa kipindi hiki cha sherehe za Pasaka.
0 comments: